machafuko yazuka zanzibar

WASIWASI mkubwa umetanda kwa siku ya pili mfululizo katika mitaa ya miji ya Zanzibar baada ya askari wa jeshi la polisi kupiga mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya wafuasi wa taasisi za kidini zinaozongozwa na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI).
Wafuasi hao ambao walikusanyika katika makao makuu ya polisi mkoa wa mjini magharibi Madema jumamosi jioni, kushindikiza kutolewa kwa viongozi wao wanaoshikiliwa kituoni hapo.
Kamishna wa jeshi la polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa aliwaambia waandishi wa habari kuwa wafuasi hao wamefanya uharibifu mkubwa ikiwa pamoja na kuchoma moto makanisa mawili na kwamba watu saba wanaotuhumiwa saba wamekamatwa na jeshi hilo.
Akizungumzia kuhusu hali hiyo ofisini kwake Ziwani Mjini Unguja Kamishna Mussa alisema kwamba jeshi lake litaendelea kuwasaka na kuwatia mikononi wote waliopanga fujo hizo pamoja na viongozi wote wa jumuiya ya Uamsho.
Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar ndio iliyohusika na kuwachochea vijana kukusanyika na kufanya uharibifu ikiwemo kuchoma moto gari, kupanga mawe barabarani na kufanya hujuma mbali mbali kinyume cha sheria. Tutaendelea kuwasaka kwa gharama zote” alisema Mussa.
Kamishna alisema kwa sasa mikusanyiko yote ya mihadhara ya kidini na vyama vya siasa lazima ipate kibali cha polisi vyenginevyo jeshi lake litatumia nguvu za ziada kutawanya mikusanyiko hiyo ili kulinda sheria za nchi, amani na utulivu.
Maeneo kadhaa na mji wa Zanzibar hasa Darajani na Michenzani ambapo muda wote ni sehemu ambazo zenye harakati nyingi za biashara jana zilikuwa zimebakia tupu kutokana na askari waliojihami kufanya doria katika mitaa yote na kuripua mabomu kila penye kikundi cha watu waliokusanyika wakinywa kahawa.
Mitaa hiyo ilikuwa imechaguliwa na mawe, matufali na magogo yaliowekwa barabarani kuziba njia kuzuwia magari yasipite huku mipira ya magari ikiwashwa moto na vijana hao.
Hata hivyo Kamishna wa Polisi alijizuwia kuhusisha harakati za Uamsho na chama cha siasa pamoja na kukataa kutaja majina ya viongozi ambao tayari wanashikiliwa na jeshi lake.
Mpaka sasa hivi sina majina yao kwa jumla lakini tumewakamata viongozi wa Uamsho na tunatendelea kuwasaka lakini jina moja tu ndio ninalo ambalo ni Mussa Abdallah Juma” alisema Kamishna huyo.



Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Bishop Dickoson Maganga alisema watu wasiojulikana walivamia kanisa lao eneo la Kariakoo Mjini Zanzibar majira ya saa 4.30 usiku na kuvunja ukuta, kuchoma viti vya plasitiki pamoja na gari yake.
Nasikitika na tukio hili ambalo tayari tumeiarifu polisi ambao jana usiku walifika hapa wakishirikiana na kikosi cha kuzima moto na kufanikiwa kuuzima moto huo ambayo kwa habati nzuri haujaathiri paa la kanisa letu” alisema kiongozi huyo.
Alisema kundi la watu ambalo lilikuwa likitoa maneno ya kashfa na kutishia maisha ya waumini waliokuwa wakifanya ibada usiku huo kukatisha ibada hiyo pamoja na kusababisha uharibifu wa mali ya kanisa hilo yenye thamani ya zaidi ya shilingi millioni mia moja.
Kutokana na hali hiyo jumuiya ya Uamsho imetoa taarifa yake kwa vyombo vya habari kwa kukanusha kuhusika na kuchochea watu kuchoma kanisa pamoja na kuharibu mali za watu.
Hata hivyo Katibu wa Jumuiya hiyo, Abdallah Said alisema katika taarifa hiyo kwamba jeshi la polisi linapaswa kubeba lawama kwa yote yaliotokea kutokana na kuvunja sheria na kuwakamata viongozi bila ya utaratibu wa busara.
Uislamu ni dini ya amani na inahimiza mashirikiano na utulivu na hatuwezi kuwatuma watu kwenda kuvunja makanisa na kuharibu mali kwa sababu ndani ya imani zetu tunajua hilo ni kosa na jambo ambalo halifai katika maarisho ya dini yetu” alisema Sheikh Abdallah.
Taarifa hiyo ilisema pia kwamba Uamsho imekuwa wazi katika kudai maslahi ya Zanzibar na sio vyenginevyo na kuahidi kufanya hivyo kwa njia za amani na iwapo watakuwa wamekosea basi wapo tayari kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Ni lazima polisi wajue kwamba tupo tayari kufanya kazi kwa misingi ya kisheria na hata kwa kujisalimisha tupo tayari lakini ukamataji busara na sheria haukubaliki na ni vigumu kwa wafuasi wetu kuwadhibiti wasilalamike, tunachokitaka ni kura ya maoni haraka na hilo tutaendelea kulidai” alisisitiza Katibu wa Jumuiya hiyo katika taarifa yake.
Wakati viongozi wa Uamsho wakiendelea kutafutwa na jeshi la polisi nyumba ya kiongozi aliyeongoza maandamano juzi Sheikh Farid Hadi Ahmed inadaiwa kuvunjwa milango usiku wa manane alipokuwa akitafutwa na jeshi la polisi.
Hata hivyo taarifa hizo zimeshindwa kuthibitishwa na jeshi la polisi iwapo ni kweli polisi ndio waliofanya kitendo hicho au laa lakini wanafamilia wanasema waligongewa milango na kutakiwa wafungue baada ya kutofungua walisikia kishindo kikubwa cha kusukumwa milango hiyo, nyumba iliyopo eneo la Mbuyuni Mjini Unguja.
Vijana katika mitaa ya Zanzibar jana walionekana wakiwa na hamasa kubwa wakidai kuendelea kuungana na viongozi wao kudai haki ya Zanzibar pamoja na kutaka Zanzibar huru kutoka ndani ya mikono ya Muungano.
Sisi tunachokitaka Zanzibar yetu watupige mabomu, watuuwe, watukamate lakini tunataka Zanzibar yetu na hatusikii lolote” Vijana walisema katika nyakati tofauti.

Comments